Ijumaa, 11 Machi 2016

LUCKY DUBE NA MTIZAMO WAKE KUHUSU WANAWAKE































Dunia nzima nadhani inamfahamu Lucky Dube ambaye ni mwanamuziki nguli wa reggae kutoka Afrika Kusini, ambaye tungo zake zimeweka rekodi kubwa kwenye muziki huo mpaka sasa anapotimiza miaka 9 tangu kuuawa kwake, baada ya kupigwa risasi na watu ambao walitaka kumuibia gari lake alipoenda kuwashusha watoto wake kwa mjomba wao.
Lucky Philip Dube alizaliwa tarehe 3 August 1964 katika eneo la Ermelo kwa sasa linajulikana kama Mpumalanga nchini Afrika Kusini akiwa ni mtoto wa kwanza kwa mama yake. Wazazi wa Lucky Dube walitengana kabla hajazaliwa, na tetesi zinasema kuwa baba yake alikuwa ni raia wa Zimbabwe, na kabla Lucky hajazaliwa alilazimika kuondoka na kurudi Zimbabwe.

Utotoni mwake Lucky Dube alilelewa sana na bibi yake kutokana na mama yake kufanya kazi nje ya mahali ambapo wanaishi ili aweze kupata kipato na kumudu hali ya maisha, Katika maisha yake Lucky Dube hakuwahi kumjua baba yake, na habari zinasema kuwa mwaka ambao familia ya baba yake ilipanga kufanya mipango ili waunganike na mtoto wao huyo, ndio mwaka ambao Lucky Dube alifariki.
Kutokana na kulelewa na bibi yake Lucky Dube alimpenda sana na kwenye moja ya mahojiano yake na vyombo vya habari, aliwahi kusema kuwa bibi yake huyo ndiye kipenzi chake bora, hii inaonyesha kiasi gani Lucky alitambua thamani ya mapenzi ya bibi yake huyo kwake, na kumpa nafasi kubwa moyoni mwake.
Ukisikiliza tungo zake Lucky Dube ameimba mambo mengi yanayogusa jamii na maisha tunayoishi, naweza sema hakuna wimbo alioimba usiguse kitu chochote kwenye maisha yako, lakini leo nataka kuzungumzia upendo wake na jinsi alivyotambua thamani ya mwanamke katika jamii, na kutunga tungo ambazo moja kwa moja zinamgusa mwanamke, ambaye alimlea kwa maisha yake yote.
Nikianza na wimbo wa “God bless the woman”, Luck Dube anaanza kwa kusema "Katikati ya usiku mkubwa, namsikia akisali kwa uchungu na ulaini, alisali kwa ajili ya watoto wake, alisali kw ajili ya elimu yao, kisha alisali kwa ajili ya mwanaume aliyemuacha na watoto" (In the middle of the night I heard her pray so bitterly, And so softly yeah...She prayed for her children, She prayed for their education, Then she prayed for the man That left her with her children)
Kwenye hii tungo Lucky Dube aliona ni jinsi gani mwanamke anajitoa nafsi yake kwa ajili ya watoto wake, akitolea mfano kusali tu, lakini hebu tujiulize, ni mangapi wanawake wanajitoa kwa ajili yetu na kupelekea kukosa muda wa kufanya mambo mengine kwa faida yao binafsi!? lakini pia mwanamke huyu huyu amejitoa na kumuombea yule ambaye amemsababisha apitie kwenye magumu ya kulea familia hii peke yake, na kumuombea. Hii inaonyesha ni jinsi gani inaonyesha wanawake pia wana huruma ya kuweza kubeba mzigo hata usio wake ili jamii yake iwe salama.
Lucky Dube kwenye tungo hiyo aliendelea kwa kusema .."Tunawasifia mashujaa kila siku, lakini kuna wale ambao tunasahau kuwasifia, wanawake wa hii dunia, hawakimbii kitu chochote, husimama na kupigania kile ambacho ni sahihi, hata nyakati ambazo ni ngumu, huwa watulivu na wenye upole, hawakimbii majukumu, husiamama na kupigania kilicho sahihi ". (We, praise heroes everyday, But there are those that we forget To praise,The women of this world. They don't run from anything,They stand and fight for what's right, Even when times are so hard, They do not run from responsibilities, They stand and fight for what Is right).
Hapa Lucky Dube amekumbusha dunia kuwa tunawasifia mashujaa kila siku, ambao labda wamefanya jambo fulani kwenye hii duni, labda nitolee mfano Mwl. Nyerere kwa Tanzania, au Nelson Mandela kwa Afrika Kusini na kwengineko duniani, lakini tunamsahau shujaa wetu wa kila siku kwenye dunia, ambaye ni mwanamke, ambaye pia huwa mvumilivu na mpole pale anapokutana na mazingira magumu katika maisha yake, anaendelea kuwa thabiti kukabiliana nayo, tutolee mfano pale mtoto anapoumwa nyakati za usiku, haijalishi njia atakayopita ni ya kutisha kiasi gani lakini mwanamke huyu lazima atathubutu kupita ili mradi mtoto wake awe salama tena.
Swali la kujiuliza hapa, ni wangapi kwenye hii dunia wanathamini mchango wa wanawake hawa na kuwapa tuzo ya heshima isiyofutika na kudumu kama hii!?
Itaendelea siku nyengine nikiendelea kuzichambua tungo zake mbali mbali na za wasanii tofauti tofauti wa muziki wa reggae.

Hakuna maoni: